| Chapter 7 |
1 | Yahusu sasa mambo yale mliyoandika: naam, ni vizuri kama mtu haoi; |
2 | lakini kwa sababu ya hatari ya uzinzi, basi, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. |
3 | Mume atimize wajibu alio nao kwa mkewe, naye mke atimize wajibu alio nao kwa mumewe. |
4 | Mke hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mumewe anayo; hali kadhalika naye mume, hana mamlaka juu ya mwili wake, bali mkewe anayo. |
5 | Msinyimane haki zenu, isipokuwa kama mnaafikiana kufanya hivyo kwa kitambo tu, ili mpate nafasi nzuri ya kusali. Kisha rudianeni tena mara, ili Shetani asije akawajaribu kwa sababu ya udhaifu wenu. |
6 | Ninayowaambieni sasa ni mawaidha, si amri. |
7 | Ningependa watu wote wawe kama mimi nilivyo; lakini kila mmoja anacho kipaji chake kutoka kwa Mungu; mmoja kipaji hiki na mwingine kile. |
8 | Basi, wale ambao hawajaoana na wale walio wajane nawaambia kwamba ni vema kuendelea kuwa kama mimi nilivyo. |
9 | Hata hivyo, kama mtu hawezi kujizuia basi, na aoe; maana ni afadhali zaidi kuoa kuliko kuwaka tamaa. |
10 | Kwa wale waliooa ninayo amri, tena si yangu, ila ni ya Bwana: mke asiachane na mumewe; |
11 | lakini kama akiachana naye, basi abaki bila kuolewa; ama la, apatanishwe na mume wake. Mume naye asimpe talaka mkewe. |
12 | Kwa wale wengine, (mimi binafsi, si Bwana) nasema hivi: Ikiwa mwanamume Mkristo anaye mke asiyeamini, na huyo mwanamke akakubali kuendelea kuishi naye, asimpe talaka. |
13 | Na, kama mwanamke Mkristo anaye mume asiyeamini, na huyo mwanamume akakubali kuendelea kuishi naye, basi, asimpe talaka mumewe. |
14 | Kwa maana huyo mume asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mkewe; na huyo mke asiyeamini hupokelewa kwa Mungu kwa kuungana na mumewe. Vinginevyo watoto wao wangekuwa si wa Mungu; kumbe sasa ni watoto wake Mungu. |
15 | Hata hivyo, ikiwa yule asiyeamini anataka kumwacha mwenzake aliye Mkristo, basi, na amwache tu. Hapo huyo Mkristo, mume au mke, atakuwa huru. Maana Mungu amewaiteni ninyi muishi kwa amani. |
16 | Wewe mama Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mume wako? Au wewe mume Mkristo, unawezaje kuwa na hakika kwamba hutaweza kumwokoa mkeo? |
17 | Kwa vyovyote kila mmoja na aishi kufuatana na vipaji alivyogawiwa na Bwana, na kama alivyoitwa na Mungu. Hili ndilo agizo langu kwa makanisa yote. |
18 | Kama mtu aliitwa akiwa ametahiriwa, basi asijisingizie kwamba hakutahiriwa; na kama alipoitwa hakuwa ametahiriwa, basi na asitahiriwe. |
19 | Maana kutahiriwa au kutotahiriwa si kitu; kilicho muhimu ni kuzishika amri za Mungu. |
20 | Basi, kila mmoja na abaki kama alivyokuwa wakati alipoitwa. |
21 | Je, wewe ulikuwa mtumwa wakati ulipoitwa? Sawa, usijali; lakini ukipata fursa ya kuwa huru, itumie. |
22 | Maana yeye aliyeitwa na Bwana akiwa mtumwa huyo huwa mtu huru wa Bwana. Hali kadhalika naye aliyeitwa akiwa mtu huru, huwa mtumwa wa Kristo. |
23 | Nyote mmenunuliwa kwa bei; kwa hiyo msiwe tena watumwa wa watu. |
24 | Ndugu zangu, kila mmoja wenu basi, na abaki na Mungu kama alivyokuwa wakati alipoitwa. |
25 | Sasa, kuhusu mabikira na waseja, sina amri kutoka kwa Bwana; lakini natoa maoni yangu mimi ambaye kwa huruma yake Bwana nastahili kuaminiwa. |
26 | Basi, kutokana na shida iliyopo sasa nadhani ingefaa mtu abaki kama alivyo. |
27 | Je, umeoa? Basi, usitake kuachana na mkeo. Wewe hukuoa? Basi, usitake kuoa. |
28 | Lakini ikiwa utaoa hutakuwa umetenda dhambi; na msichana akiolewa hatakuwa ametenda dhambi. Hao watakaooana watapatwa na matatizo ya dunia hii, lakini mimi ningependa hayo yasiwapate ninyi. |
29 | Ndugu, nataka kusema hivi: muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa na waishi kama vile hawakuoa; |
30 | wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu; |
31 | nao wenye shughuli na dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu, kama tuujuavyo, unapita. |
32 | Ningependa ninyi msiwe na wasiwasi. Mtu asiye na mke hujishughulisha na kazi ya Bwana jinsi atakavyompendeza Bwana. |
33 | Mtu aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia jinsi atakavyompendeza mkewe, |
34 | naye amegawanyika. Mwanamke asiyeolewa au bikira hujishughulisha na mambo ya Bwana apate kujitolea mwili na roho kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii jinsi atakavyompendeza mumewe. |
35 | Nawaambieni haya kwa faida yenu, na si kwa kuwawekeeni kizuio. Nataka tu muwe na mpango unaofaa, mpate kumtumikia Bwana kwa moyo na nia moja. |
36 | Kama mtu anaona kwamba hamtendei vyema mchumba wake asipomwoa, na kama tamaa zake zinamshinda, na afanye atakavyo; waoane tu; hatakuwa ametenda dhambi. |
37 | Lakini kama huyo mwanamume akiamua kwa hiari moyoni mwake kutooa na kama anaweza kuzitawala tamaa zake na kuamua namna ya kufanya, basi, anafanya vizuri zaidi asipomwoa huyo mwenzake bikira. |
38 | Kwa maneno mengine: yule anayeamua kumwoa huyo mchumba wake anafanya vema; naye anayeamua kutomwoa anafanya vema zaidi. |
39 | Mwanamke huwa amefungwa na mumewe kwa muda wote mumewe aishipo. Lakini mumewe akifa, mama huyo yuko huru, na akipenda anaweza kuolewa na mtu yeyote, mradi tu iwe Kikristo. |
40 | Lakini, nionavyo mimi, atakuwa na heri zaidi kama akibaki hivyo alivyo. Hayo ni maoni yangu, na nafikiri mimi pia ninaye Roho wa Mungu. |